Bondia Francis Miyeyusho (kulia) akimtupia konde mpinzani wake, Joshua Amakulu . Picha na MWANANCHI
|
Bondia, Francis ‘Chichi mawe’ Miyeyusho juzi usiku aliibuka kinara baada ya kumgaragaza Joshua Amukulu wa Kenya kwa Knock Out (KO) raundi ya pili ya pambano la raundi nane la uzani wa light. Katika pambano hilo lililopigwa kwenye Ukumbi wa Msasani Club jijini Dar es Salaam, Miyeyusho alionekana yuko imara tangu kengele ya kuashiria kuanza kwa raundi ya kwanza ya pambano hilo.
Amukulu ndiye alikuwa wa kwanza kurusha konde katika raundi hiyo na Miyeyusho kukwepa na kujibu mashambulizi yaliyodumu hadi dakika tatu za raundi ya kwanza zinamalizika.
Hali ilikuwa tete kwa Amukulu raundi ya pili ya pambano hilo ambapo kabla ya kengele ya kuashiria kumalizika kwa dakika tatu za raundi hiyo, konde la Miyeyusho lilimpotezea mwelekeo mpinzani wake ambaye alishindwa kuendelea na pambano na mwamuzi kutoa ushindi wa KO kwa Miyeyusho.
“Ni matokeo ambayo niliyatarajia kutokana na maandalizi niliyofanya, nilisema tangu mwanzo kuwa ‘hapa lazima ukae’ ndivyo ilivyokuwa kwa huyu Mkenya, hili ni fundisho kwa mabondia wengine pia,” alitamba Miyeyusho.
0 comments: